Saudi Arabia yakaidi shinikizo la Marekani kuhusu Israel
Saudi Arabia imesisitiza kuwa haitaanzisha mahusiano rasmi ya kidiplomasia na Israel hadi kuwepo kwa “njia isiyoweza kurudishwa nyuma” kuelekea kuundwa kwa taifa huru la Palestina.
Kauli hiyo imekuja kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa Saudi Arabia kuhusu juhudi za kupanua makubaliano ya Abraham Accords na kuimarisha ushirikiano wa kikanda Mashariki ya Kati.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema msimamo wa nchi hiyo kuhusu Palestina bado haujabadilika, ikisisitiza kuwa suluhisho la mataifa mawili ndilo sharti muhimu kabla ya hatua yoyote ya kuhalalisha uhusiano na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa za Reuters, Riyadh inataka hatua za wazi na za kudumu kuelekea kuanzishwa kwa taifa la Palestina lenye mamlaka kamili kabla ya kujiunga rasmi na Abraham Accords zilizowekwa mwaka 2020 chini ya uongozi wa Trump.
Msimamo huo umejiri wakati Marekani ikiendelea kushinikiza mataifa ya Kiarabu kuanzisha mahusiano rasmi na Israel, licha ya vita vinavyoendelea Gaza na kuongezeka kwa hasira katika mataifa ya Kiarabu kuhusu hali ya Wapalestina.
Wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati wanasema Saudi Arabia inajaribu kusawazisha uhusiano wake wa kimkakati na Marekani pamoja na shinikizo la ndani kutoka kwa wananchi wanaounga mkono Palestina.
