Aliyekuwa Rais wa Korea Kusini ahukumiwa miaka 30 jela
Mahakama Kuu ya Wilaya ya Kati ya Seoul (Seoul Central District Court) imemhukumu aliyekuwa Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, kifungo cha miaka 30 jela siku ya Ijumaa baada ya kupatikana na hatia katika kesi iliyohusisha matumizi mabaya ya mamlaka na kuhatarisha usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa Mahakama, Yoon alitoa maagizo ya siri ya kuendesha operesheni ya kijeshi iliyohusisha ndege zisizo na rubani kuvuka mpaka kuelekea North Korea. Mahakama ilieleza kuwa hatua hiyo ilifasiriwa kama jaribio la makusudi la kuibua mgogoro wa usalama kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kuunda mazingira ya kisiasa yaliyokuwa na manufaa kwake.
Katika uamuzi wake, Mahakama ilisema operesheni hiyo ilikuwa sehemu ya mpango mpana uliolenga kuandaa mazingira ya kisiasa yaliyosaidia jaribio la kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba mwaka 2024. Jaribio hilo lilizua mjadala mkubwa wa kisiasa nchini South Korea na kusababisha wasiwasi miongoni mwa wananchi, wawekezaji na wadau wa uchumi.
Mahakama pia ilibainisha kuwa matendo hayo yalikiuka misingi ya utawala wa sheria na kuhatarisha uthabiti wa taasisi za kidemokrasia za taifa. Majaji walieleza kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwajibika kwa vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa na utulivu wa nchi.
Hukumu hiyo ya miaka 30 jela inatajwa kuwa moja ya hukumu nzito zaidi kuwahi kutolewa dhidi ya kiongozi wa zamani wa Korea Kusini, huku ikionyesha msimamo wa mfumo wa mahakama wa kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi wa juu wa serikali bila kujali nafasi walizowahi kushika.
Uamuzi huo unatarajiwa kuendelea kuvuta hisia za wananchi na wachambuzi wa siasa ndani na nje ya Korea Kusini kutokana na athari zake kwa historia ya kisiasa ya taifa hilo pamoja na uhusiano wake wa kiusalama na Korea Kaskazini.
