Trump aongeza muda wa kusitisha mashambulizi dhidi ya Iran
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuongeza muda wa kusitisha mashambulizi dhidi ya Iran bila kuweka kikomo maalum, hatua iliyochochewa na ombi kutoka kwa viongozi wa Pakistan.
Kupitia ujumbe wake aliouandika mtandaoni, Trump amesema alipokea maombi kutoka kwa Mkuu wa Majeshi wa Pakistan, Asim Munir, pamoja na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, wakimtaka apeane muda ili Iran iweze kujipanga na kuwasilisha msimamo wa pamoja kwa ajili ya mazungumzo ya amani.
Ameeleza kuwa hali ya kisiasa ndani ya Iran inaonekana kuwa na mgawanyiko, hivyo kusitishwa kwa mashambulizi kunalenga kutoa nafasi kwa viongozi wa taifa hilo kukubaliana kwanza kabla ya kuingia kwenye mazungumzo rasmi.
Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi kulegeza ulinzi au maandalizi ya kijeshi, akibainisha kuwa majeshi ya Marekani bado yako tayari kuchukua hatua wakati wowote endapo hali itabadilika.
Ameongeza kuwa kusitishwa huko kutaendelea hadi pale Iran itakapowasilisha pendekezo rasmi na mazungumzo ya amani kufikia hatua inayoridhisha.
Awali, akizungumza na kituo cha CNBC, Trump alinukuliwa akisema kuwa Marekani ilikuwa tayari kabisa kuanza operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran, akionyesha kuwa maandalizi ya mashambulizi yalikuwa tayari yamekamilika.
Uamuzi huu umeibua mjadala mkubwa kimataifa, huku ukitazamwa kama hatua ya kutoa nafasi kwa diplomasia, lakini pia ukiwaacha wengi wakisubiri kuona hatua itakayofuata baada ya kipindi hiki cha kusitisha mashambulizi.
