NEWS

China: Mawaziri wa zamani wa ulinzi wahukumiwa kifo kwa rushwa

Mahakama ya kijeshi nchini China imewahukumu kifo mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi, Wei Fenghe na Li Shangfu, baada ya kupatikana na hatia ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Hukumu hiyo iliyotangazwa kupitia vyombo vya habari vya serikali ya China, imesitishwa kwa miaka miwili, ambapo baada ya kipindi hicho adhabu zao zitabadilishwa kuwa kifungo cha maisha bila nafasi ya msamaha au kupunguziwa adhabu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, viongozi hao walihusishwa na kupokea kiasi kikubwa cha rushwa na kutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi pamoja na kuwapa wengine upendeleo usio halali. Mali zao zote binafsi zimechukuliwa na serikali.

Li Shangfu alihudumu kama Waziri wa Ulinzi kuanzia Machi 2023 kabla ya kuondolewa Oktoba mwaka huo, wakati Wei Fenghe alihudumu kuanzia 2018 hadi 2023 kabla ya kurithiwa na Li.

Hukumu hizo zinatajwa kuwa sehemu ya kampeni kubwa ya kupambana na rushwa inayoendelea nchini China chini ya Rais Xi Jinping, ingawa baadhi ya wachambuzi wanaiona pia kama kampeni yenye mwelekeo wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *