Zimbabwe yapitisha muswada wa kuongeza mihula ya uongozi
Bunge la Jamhuri ya Zimbabwe limepitisha hatua ya kwanza ya usomaji wa muswada wenye utata mkubwa unaolenga kufanya marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo, ambapo mabadiliko hayo yanaweza kuongeza muda wa mihula ya uongozi wa Rais na Wabunge kutoka miaka mitano hadi miaka saba.
Muswada huo pia unapendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa uchaguzi wa Rais, ambapo badala ya wananchi kumpigia kura moja kwa moja kiongozi wa taifa, jukumu hilo linaweza kuhamishiwa Bungeni, hatua inayozua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini humo.
Baadhi ya vifungu vilivyomo katika mapendekezo hayo vinadaiwa kufungua njia ya kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa pamoja na Wabunge waliopo madarakani kuendelea kushika nafasi zao hadi mwaka 2030, jambo ambalo limezua hisia tofauti ndani na nje ya nchi.
Mapendekezo hayo tayari yameibua upinzani mkali kutoka kwa makundi mbalimbali, yakiwemo vyama vya wanasheria nchini humo ambavyo vimesema kuwa mabadiliko hayo yanaweza kudhoofisha taasisi za kidemokrasia na kuongeza mkusanyiko wa madaraka mikononi mwa viongozi wachache.
Aidha, taasisi za kidini pamoja na mashirika yanayotetea haki za binadamu yameeleza wasiwasi wao, yakisisitiza kuwa marekebisho hayo yanapaswa kufanyika kwa kufuata utaratibu wa kura ya maoni ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa moja kwa moja katika maamuzi hayo muhimu.
Kwa sasa, muswada huo unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili siku ya Jumatano, ambapo wabunge watapata nafasi ya kujadili marekebisho zaidi ya kumi yaliyopendekezwa kabla ya hatua ya kupigiwa kura.
Ili kupitishwa rasmi, muswada huo utahitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya kura katika mabunge yote mawili ya nchi, hatua inayofanya mchakato huo kuwa na changamoto kubwa ya kisiasa na kisheria.
