NEWS

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ajiuzulu madarakani

Waziri Mkuu wa Uingereza na kiongozi wa Chama cha Labour, Keir Starmer, ametangaza rasmi kujiuzulu kutoka nafasi zake zote mbili baada ya kuhudumu madarakani kwa takriban miaka miwili.

Starmer ametangaza uamuzi huo akiwa nje ya makazi rasmi ya Waziri Mkuu katika 10 Downing Street, akisisitiza kuwa katika kipindi chote cha uongozi wake, kila uamuzi aliouchukua ulilenga kulinda na kuweka mbele maslahi ya taifa la Uingereza.

“Nimefanya kila uamuzi nikiwa na lengo la kuweka mbele maslahi ya nchi ninayoipenda,” alisema Starmer.

Katika hotuba yake iliyojaa hisia na iliyogusa hisia za wengi, Starmer alitumia nafasi hiyo kumshukuru mke wake, Vic, kwa kuwa msaada mkubwa katika kipindi chote cha uongozi wake, akimtaja kama nguzo muhimu iliyompa nguvu katika nyakati ngumu na zenye changamoto.

“Nataka kumshukuru mke wangu wa ajabu, Vic, ambaye amekuwa mwamba wangu katika kila hatua ya safari hii. Pia nataka kuwa baba bora kwa watoto wangu wazuri,” aliongeza.

Starmer pia alieleza kuwa moja ya sababu za uamuzi wake ni kutaka kutumia muda zaidi na familia yake baada ya miaka ya majukumu mazito ya uongozi wa taifa.

Kujiuzulu kwake kunafungua ukurasa mpya katika siasa za Uingereza, huku Chama cha Labour kikitarajiwa kuanza mchakato wa ndani wa kumpata kiongozi mpya atakayechukua nafasi ya uongozi wa chama na ofisi ya Waziri Mkuu.

Wachambuzi wa siasa wanasema hatua hiyo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika mwelekeo wa kisiasa wa Uingereza, hasa katika kipindi ambacho nchi hiyo inaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *