NEWS

Australia yateua mwanamke kuongoza Jeshi kwa mara ya kwanza

Serikali ya Australia imetangaza uteuzi wa Luteni Jenerali Susan Coyle kuwa Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo, hatua ya kwanza ya aina yake tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo zaidi ya miaka 125 iliyopita.

Coyle anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Julai 2026, akichukua nafasi ya Jenerali Simon Stuart. Uteuzi wake unatajwa kufanyika wakati jeshi hilo likikabiliana na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia na masuala ya ubaguzi ndani ya vikosi vyake.

Waziri Mkuu Anthony Albanese amesema uteuzi huo ni alama muhimu ya mabadiliko ndani ya jeshi na unaweza kusaidia kufungua nafasi zaidi kwa wanawake kujiunga na kupanda vyeo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi Richard Marles ameuelezea uteuzi huo kama hatua kubwa ya maendeleo, akibainisha kuwa mafanikio ya Coyle yatachochea motisha kwa wanawake waliopo jeshini na wanaotarajia kujiunga baadaye.

Kwa sasa, wanawake wanachangia takriban asilimia 21 ya wanajeshi wote na asilimia 18.5 ya nafasi za uongozi wa juu, huku serikali ikilenga kufikia asilimia 25 ifikapo mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *