NEWS

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ang’oka madarakani

Baraza la Nchi Wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) limepiga kura ya kumuondoa madarakani Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo, Karim Khan, kufuatia tuhuma za utovu wa nidhamu wa kingono.

Uamuzi huo umechukuliwa takribani miaka miwili baada ya tuhuma dhidi ya Khan kuibuka. Hata hivyo, timu yake ya wanasheria imepinga hatua hiyo, ikidai kuwa kuondolewa kwake kumechochewa na sababu za kisiasa.

Tayab Ali, kiongozi wa timu ya mawakili wa Khan, amesema jopo la majaji lilihitimisha kwa kauli moja kuwa uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Usimamizi wa Ndani (OIOS) haukuthibitisha kuwapo kwa utovu wa nidhamu wala ukiukwaji wa wajibu kwa Khan.

Ali amesema uamuzi wa kumuondoa Khan haukuzingatia ushahidi wala hitimisho la majaji huru waliolichunguza suala hilo, akisisitiza kuwa uhuru wa ICC unapaswa kulindwa dhidi ya maamuzi yanayochochewa na siasa.

Khan, ambaye ni raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 56, amekanusha tuhuma zote dhidi yake. Mwanamke aliyetoa tuhuma hizo, aliyetambulishwa kwa jina la Sarah pekee, alidai kuwa Khan alionyesha tabia ya kumgusa kimapenzi bila ridhaa yake.

Kabla ya kuondolewa rasmi, Khan alikuwa amejiondoa kwa muda katika nafasi yake tangu Juni, baada ya jopo la usimamizi kubaini kuwa alihusika na kile kilichoelezwa kuwa ni “utovu mkubwa wa nidhamu.”

Tukio hilo linatokea wakati ICC ikiendelea kukabiliwa na shinikizo kutoka Marekani na Israel, hasa baada ya Khan kuomba hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Yoav Gallant, mwaka 2024.

Kwa sasa, ICC imetangaza kuwa ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu itaongozwa kwa muda na Manaibu Waendesha Mashtaka Nazhat Shameen Khan na Mame Mandiaye Niang.

Kuondolewa kwa Karim Khan kumeanzisha rasmi mchakato wa kumpata Mwendesha Mashtaka Mkuu mpya wa ICC, ingawa kura ya kumchagua mrithi wake haitarajiwi kufanyika kabla ya mwaka ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *