SPORTS

FIFA kuanza tathmini ya pendekezo la kuongeza timu 64 Kombe la Dunia

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amesema pendekezo la kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia kutoka 48 hadi 64 litafanyiwa tathmini baada ya kumalizika kwa michuano ya mwaka 2026.

Infantino amesema mafanikio ya mfumo mpya wa timu 48 katika Kombe la Dunia 2026 yatakuwa sehemu muhimu ya kuamua kama upanuzi wa mashindano hayo hadi timu 64 utawezekana na kama utakuwa na mchango chanya katika maendeleo ya soka duniani.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Blue Sport cha Uswisi, Infantino amesema mjadala kuhusu kuongeza idadi ya timu utafanyika baada ya mashindano ya mwaka 2026, akieleza kuwa lengo la Kombe la Dunia ni kuwa mashindano yanayowakutanisha wawakilishi wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Pendekezo hilo liliwasilishwa rasmi mwezi Aprili 2025 na Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL), likitaka idadi ya timu iongezwe hadi 64 kuanzia Kombe la Dunia la mwaka 2030. Hata hivyo, FIFA bado haijatoa uamuzi wa mwisho kuhusu mpango huo.

Kombe la Dunia 2030 limepangwa kufanyika kwa ushirikiano wa Hispania, Ureno na Morocco, huku Argentina, Uruguay na Paraguay zikipangwa kuwa mwenyeji wa mechi tatu za ufunguzi kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 1930 nchini Uruguay.

Pamoja na pendekezo hilo kuwa na wafuasi, limeendelea kukutana na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa soka duniani.

Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Aleksander Ceferin, amelipinga wazo hilo akisema linaweza kuwa na athari mbaya kwa mustakabali wa mashindano hayo pamoja na mfumo wa kufuzu.

Naye Rais wa Shirikisho la Soka la Asia (AFC), Sheikh Salman bin Ibrahim Al Khalifa, amesema kuongeza zaidi idadi ya timu kunaweza kusababisha changamoto kubwa katika uendeshaji wa mashindano na kuleta ugumu katika kupanga ratiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *