NEWS

Bei ya mafuta yashuka baada ya makubaliano ya Marekani na Iran

Mataifa mbalimbali duniani yameanza kupumua kwa ahueni baada ya kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia, kufuatia matumaini ya kupungua kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.

Hali hiyo inatokana na taarifa za Marekani na Iran kufikia makubaliano ya awali ya kusitisha uhasama na kurejesha kwa ufanisi shughuli za usafirishaji wa nishati kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi duniani.

Kwa mujibu wa taarifa za masoko ya nishati, bei ya pipa moja la mafuta ghafi imepungua hadi takribani dola 78 leo Jumanne, ikilinganishwa na karibu dola 120 zilizorekodiwa miezi miwili iliyopita wakati wa kilele cha mvutano huo.

Wachambuzi wa uchumi wanasema kushuka kwa bei hiyo kunatoa nafuu kwa masoko ya kimataifa, hasa baada ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuonya kuwa bei kubwa ya mafuta ilikuwa tishio kwa ustawi wa nchi zinazoendelea.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa yanayoiwemo Rwanda na Tanzania yameendelea kukumbwa na athari za kupanda kwa gharama za nishati, ambapo bei ya mafuta iliripotiwa kupanda kwa zaidi ya asilimia 50 kufuatia machafuko yaliyotokea mapema mwaka 2026.

Wataalamu wa uchumi wanasema mwenendo wa sasa wa bei utategemea uimara wa makubaliano ya kisiasa kati ya mataifa hayo mawili pamoja na hali ya usalama katika njia kuu za usafirishaji wa mafuta duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *