NEWS

TRA yavunja rekodi ukusanyaji mapato

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika historia mpya baada ya kukusanya shilingi trilioni 3.58 katika mwezi Machi 2026 pekee, kiwango kinachowakilisha ufanisi wa asilimia 107.6 ya lengo lililokuwa limepangwa.

Makusanyo hayo yamechochea mafanikio makubwa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha (Januari hadi Machi 2026), ambapo TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 9.31. Hii ni ongezeko la asilimia 23.6 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita, ishara ya ukuaji thabiti wa mapato ya ndani.

Sababu kubwa ya mafanikio hayo imeelezwa kuwa ni maboresho ya mifumo ya kidijitali ndani ya taasisi hiyo. Mfumo mpya wa kodi za ndani (IDRAS), ulioanza kutumika Februari 2026, umewezesha kusajili zaidi ya walipakodi wapya 69,000 pamoja na kuunganisha taasisi 92, hatua iliyoongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wa forodha, matumizi ya mfumo wa TANCIS yameimarisha udhibiti wa mapato na kuongeza kasi ya uondoshaji wa mizigo katika vituo mbalimbali nchini, hali iliyopunguza mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

Akizungumzia mafanikio hayo, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kukuza ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia mahusiano mazuri kati ya TRA na walipakodi.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, TRA imefanikiwa kuvuka malengo yake ya ukusanyaji kwa miezi 21 mfululizo tangu Julai 2024, hatua inayoonyesha kuimarika kwa nidhamu ya ulipaji kodi pamoja na kuboreka kwa mazingira ya biashara nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *